Mwanaume wa miaka 50 alalaye kichakani kwa miaka mitano, sasa aomba msaada wa kujengewa nyumba
Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 50 kutoka mtaa wa Athena katika Kaunti Ndogo ya Thika Magharibi, amekuwa akiishi kichakani kwa zaidi ya miaka mitano kutokana na umasikini uliomkosesha makazi ya kudumu.
Dominic Mwangi, anayejulikana kwa jina la utani kama “Msanii”, aliacha masomo akiwa darasa la saba na hana mafunzo yoyote ya kiufundi wala ajira ya kudumu.
Anasema maisha yake ya kuishi nje yalianza baada ya kushindwa kujenga nyumba kwenye kipande cha ardhi alichopewa na marehemu baba yake.
“Niligawiwa ardhi kama ndugu zangu, lakini sikuwa na uwezo wa kujenga nyumba. Nilikuwa sina pesa,” anasema Mwangi.
Wakati wa mvua, hujikinga kwa kutumia mifuko ya nailoni ya zamani au hujificha ndani ya shimo alilochimba ambalo awali lilinuia kuwa choo cha nje.
Mkewe alimwacha na kuondoka na watoto wao wawili baada ya kushindwa kuvumilia ugumu wa maisha aliyokuwa akiishi.
Marafiki wake waliwahi kujaribu kumjengea kibanda cha matofali, lakini kiliporomoka kabla ya kukamilika kutokana na mvua kubwa.
Kwa sasa, anaishi katika mazingira hatarishi yaliyojaa wanyama wa porini kama fisi na nyoka, hali iliyomlazimu kuomba msaada kutoka kwa wahisani.
“Nahitaji tu nyumba ndogo, vyombo vya matumizi ya nyumbani ili niweze kuanza maisha upya, na kazi yoyote ya kawaida ili nijikimu kimaisha,” aliongeza.
Majirani na jamaa zake pia wameungana naye kuomba jamii na viongozi wajitokeze kumsaidia.
Baada ya kusikia kuhusu hali yake, MCA wa eneo hilo Kennedy Mwangi, almaarufu “Kentams”, aliahidi kumjengea nyumba ya kudumu yenye maji na umeme.
“Nitahakikisha pia anapata kazi ili aishi kwa heshima kama binadamu mwingine yeyote,” alisema MCA Kentams.
Kisa hiki kimezua hisia kali miongoni mwa wakazi wa Thika, wengi wao wakitoa wito kwa serikali ya kaunti na mashirika ya kijamii kumsaidia Mwangi kurudi katika maisha ya utu.
Kwa yeyote anayetaka kumsaidia, tafadhali wasiliana na timu ya 3T TV kupitia nambari 0777 994 807, uwasiliane na uongozi/chifu wa eneo hilo au ofisi ya MCA Kennedy Mwangi.
Pata maelezo zaidi na video hapa
No comments: