Familia za Wanjiku Thiga na Peter Karanja Zaitaka Serikali Kuwaachilia Huru Mara Moja
Hali ya sintofahamu imezidi kuongezeka katika Kaunti ya Kiambu kufuatia kukamatwa na kuzuiliwa kwa viongozi wawili wa vijana, Wanjiku Thiga na Peter Karanja, huku familia zao zikishinikiza kuachiliwa kwao mara moja bila masharti.
Wanjiku Thiga, ambaye ni Mratibu wa Kitaifa wa Vijana wa Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), pamoja na Peter Karanja, kiongozi maarufu wa vijana katika Kaunti ya Kiambu, walikamatwa Jumanne kwa mazingira yasiyoeleweka, jambo lililozua maswali mengi.
Wakizungumza na wanahabari nje ya Kituo cha Polisi cha Ruiru, ambako wawili hao wanadaiwa kuzuiliwa, Simon Mwangi, kaka yake Wanjiku, alilaani vikali kukamatwa kwao na kukitaja kuwa ni kisiasa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Hii si tu kukamatwa, bali ni utekaji,” alisema Mwangi. “Hatujui kwa nini walichukuliwa na tumenyimwa haki ya kuwaona. Hii ni kinyume na katiba.”
Familia zinadai kuwa hakuna mashtaka rasmi yaliyotangazwa dhidi ya wawili hao, na juhudi za kupata taarifa kutoka kwa maafisa wa polisi zimegonga mwamba, zikiambatana na vitisho.
Fuata kiungo hiki kutazama habari kamili:
Mashirika ya kijamii na wanaharakati wa haki za binadamu pia wameonyesha wasiwasi wao, wakitoa wito kwa mamlaka kuheshimu haki za kikatiba na kuhakikisha kuwa utaratibu wa sheria unafuatwa.
Makundi ya vijana na wanaharakati sasa wameungana na familia hizo katika kutoa wito wa kuachiliwa kwao, huku baadhi yao wakitishia kuandaa maandamano ya amani iwapo serikali haitatoa mwelekeo wa wazi kuhusu suala hilo.
Kadri presha inavyozidi kuelekezwa kwa polisi na maafisa wa serikali, Wakenya wengi wanafuatilia kwa makini tukio hili, wakiwa na hofu kuwa visa vya aina hii vinaweza kuwa dalili ya kuzorota kwa uhuru wa kisiasa na kukandamizwa kwa sauti za vijana nchini.
No comments: