Maumivu Pampuni: Bei Ya Mafuta Yapanda Tena Kwa Zaidi Ya Shilingi 8


Wakenya wameamka kwa habari mbaya baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) kutangaza ongezeko kubwa la bei ya mafuta, hatua ambayo imeongeza mzigo kwa wananchi waliokuwa tayari wakikabiliana na gharama ya juu ya maisha.

Katika tangazo lake la hivi punde, EPRA imepandisha bei ya Petroli ya Super kwa KSh 8.99, Diseli kwa KSh 8.67, na Mafuta Taa (Kerosene) kwa KSh 9.65 kwa kila lita, kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Julai 15, 2025, kwa kipindi cha siku 30 zijazo.

Katika Jiji la Nairobi, bei mpya ni kama ifuatavyo: 

Petroli ya Super: KSh 186.31 kwa lita

Diseli: KSh 171.58 kwa lita

Mafuta Taa: KSh 156.58 kwa lita

Ongezeko hili linatarajiwa kusababisha mfumuko wa bei katika sekta nyingi, hasa usafiri, vyakula na bidhaa muhimu, na kuongeza shinikizo kwa familia nyingi ambazo tayari zinakabiliana na hali ngumu ya kiuchumi.

Kulingana na EPRA, ongezeko hilo limezingatia Kifungu cha 101(y) cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2019 pamoja na Notisi ya Kisheria Na. 192 ya mwaka 2022, inayotoa mwongozo wa mapitio ya bei ya mafuta kila mwezi.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya ongezeko hili linatokana na masharti mapya ya ushuru yaliyoainishwa katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2023, Marekebisho ya Sheria za Ushuru ya mwaka 2024 na ushuru wa bidhaa uliorekebishwa kutokana na mfumuko wa bei chini ya Notisi ya Kisheria Na. 194 ya mwaka 2020. Bei hizo pia zinajumuisha VAT ya asilimia 16.

Wananchi wengi wameelezea hasira zao kupitia mitandao ya kijamii, wakilalamikia ongezeko hilo na kuhoji sababu za kuendelea kubebeshwa mzigo mkubwa wa kodi. Kwa wananchi wa maeneo ya mashambani na mitaa ya kipato cha chini, athari ni kubwa zaidi, hasa kwa kuwa mafuta ya taa, yanayotegemewa kwa kupikia na taa, yamepanda kwa karibu shilingi 10 kwa lita.

Baadhi ya wananchi wamelalamika kuwa serikali hupunguza bei ya mafuta kwa kiwango kidogo sana, lakini inapofikia ongezeko, hatua hiyo huchukuliwa kwa kiasi kikubwa.

"Serikali ikipunguza bei ya mafuta hupunguza kwa shilingi moja tu, lakini wakiongeza, wanaongeza kwa shilingi tisa. Huko ni kutuchezea akili na kuhadaa Wakenya," kaandika Mkenya mmoja kwenye Mitandao ya Kijamii.

Katika mitaa ya Nairobi, Thika, Nakuru na maeneo mengine ya nchi, wananchi walifurika kwenye mitandao na mitaani kuelezea uchungu wao na kukosa matumaini.Waendesha bodaboda, wafanyabiashara wadogo na wakulima pia wanatarajiwa kupata athari kubwa, kwani mafuta ni kiungo muhimu katika mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa.

Kuna uwezekano waendeshaji wa matatu na mabasi wataanza kuongeza nauli, hasa katika maeneo ya mijini kulingana na umbali wa safari na eneo la huduma.

Kwa familia zinazotegemea mafuta ya taa kupika, hali ni mbaya zaidi. Wakati huo huo, wachuuzi na wauzaji wa bidhaa sokoni wanahofia pia bei za bidhaa muhimu kama unga, sukari, mboga na vyakula vya rejareja huenda zikapanda kutokana na gharama ya usafirishaji na usindikaji kuongezeka.

Wachumi wameonya kuwa iwapo bei za kimataifa za mafuta zitaendelea kutokuwa thabiti na kiwango cha ushuru wa ndani kitaendelea kuwa juu, Wakenya wanapaswa kujitayarisha kwa ongezeko zaidi la bei za mafuta katika miezi ijayo.

No comments:

Post a Comment